Kwa mujibu wa idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, vikosi vya mamluki na wanamgambo raia wanaohusiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain vimeweka mzingiro mkali wa kiusalama katika mji wa Al-Duraz na kwa wiki ya hamsini na saba mfululizo wamewazuia raia wa Kishia kuswali Swala ya Ijumaa ya pamoja.
Vikosi vya kijeshi, magari ya kivita na askari waliokuwa na silaha nzito walitanda kuanzia asubuhi ya Ijumaa, tarehe 7 Novemba 2025, katika maeneo yanayozunguka Msikiti wa Imam Sadiq (a.s), ili kujiandaa kukabiliana na maandamano yoyote ya wananchi watakaoonesha upinzani dhidi ya mzingiro wa kidini, kuiunga mkono Ghaza, au kupinga uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.
Katika maeneo kadhaa ya Bahrain, wananchi waliandamana kwa hasira kupinga mzingiro wa kiusalama uliowekwa nchini humo na kuonesha upinzani wao dhidi ya hatua ya utawala uliopo madarakani kuwazuia raia wa Kishia kutekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa.
Waandamanaji walisisitiza kukataa udhibiti wa serikali juu ya mambo ya kidini na kulaani vizuizi vinavyoendelea dhidi ya uhuru wa kidini, wakitoa wito wa kukomesha sera ya mateso ya kimadhehebu na mzingiro unaoathiri ibada za Waislamu wa Kishia.
Washiriki pia walisisitiza juu ya ulazima wa kuwaachilia mara moja wafungwa wa kisiasa, kutoa msamaha wa jumla kwa wafungwa wote, na kukomesha sera ya “kifo cha taratibu kilichopangwa” dhidi ya wafungwa.
Walilaani uvunjaji wa haki za kimadhehebu unaofanywa katika Gereza Kuu la Jau, pamoja na matusi ya aibu yanayolenga itikadi za Kishia, na wakaonesha upinzani kamili dhidi ya uvamizi wa wazi kwa dini na madhehebu, pamoja na kampeni rasmi zilizoandaliwa kwa lengo la kufuta utambulisho na asili ya kitaifa.
Waandamanaji pia walilaani mzingiro unaoendelea wa Wazayuni dhidi ya watu wa Ghaza na vita vya njaa vinavyoendelea katika eneo hilo licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano, na wakaitaka serikali ya Bahrain kusitisha urasimishaji wa uhusiano na utawala wa Kizayuni, kumfukuza balozi wa uvamizi na kufunga ubalozi wake mjini Manama.
Walisisitiza msimamo wao wa kuunga mkono mhimili wa muqawama huko Lebanon, Ghaza, Yemen na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na uaminifu wao kwa Shahidi wa Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrallah.
Maoni yako